Mkutano wa 17 wa Kilele wa Kundi la Nchi 20 (G20) leo Novemba 16 unaendelea kiswani Bali, Indonesia, ambapo Rais wa China Xi Jinping ametoa hotuba kwenye mkutano huo.
Akizungumzia mageuzi ya kidijitali, Rais Xi amebainisha kuwa uchumi wa dijitali kwa sasa unaendelea kupanuka, huku mageuzi ya kidijitali yakiendelea kushika kasi kote duniani, jambo ambalo limekuwa athari kubwa katika muundo wa uchumi wa dunia. Amesema katika miaka ya hivi karibuni, kundi la G20 lilifikia mwafaka kuhusu kukumbatia mageuzi ya kidijitali na kukuza uchumi wa dijitali, na limeendeleza zaidi ushirikiano kwenye nyanja hii. Rais Xi ametoa mwito kwa pande mbalimbali kutia nguvu ya msukumo kwenye ushirikiano wa kidijitali, ili kuuwezesha uchumi wa dijitali kunufaisha watu wa nchi mbalimbali.
Ili kufanikisha lengo hili, Rais Xi ametoa mapendekezo matatu, ambayo ni kushikilia mfumo wa pande nyingi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kutoa kipaumbele katika maendeleo na kuziba pengo lililopo kwenye nyanja ya dijitali, na tatu, ni kuchochea msukumo unaotokana na uvumbuzi na kuchangia ufufukaji wa uchumi kutoka kwenye athari za janga la Corona.
Mkutano huo umepitisha Azimio la Mkutano wa Kilele wa Bali wa G20.