Xi akutana na marais wa Afrika Kusini na Senegal pembeni ya mkutano wa G20
2022-11-16 10:06:26| CRI

Rais Xi Jinping wa China Jumanne mchana kwa nyakati tofauti alikutana na wenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na wa Senegal Macky Sall pembeni ya mkutano wa kundi la nchi 20 unaofanyika huko Bali Indonesia.

Akiongea na rais Ramaphosa, Xi Jinping amesema China na Afrika Kusini zina urafiki wa kipekee wa "makomredi na undugu," na kwamba kama nchi kubwa zinazoendelea, nchi hizo mbili zinatetea kithabiti usawa na haki ya kimataifa na maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea.

Naye Ramaphosa kwa mara nyingine tena amempongeza Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, na kuishukuru China kwa msaada wake wa thamani kwa Afrika Kusini na nchi nyingine za Afrika katika kukabiliana na COVID-19 na kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuzisaidia nchi za Afrika kupunguza tatizo la madeni.

Akiongea na rais wa Senegal Macky Sall, rais Xi alisema China na Senegal ni washirika muhimu na wenyeviti wenza wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). China iko tayari kuendelea kuungana na Senegal ili kusonga mbele katika kutafuta maendeleo na ufufuaji, na kusaidiana katika masuala ya mamlaka, usalama na maslahi makuu ya maendeleo. Naye rais Sall aliishukuru China kwa msaada wake muhimu kwa Senegal na nchi nyingine za Afrika, na kwa kuwa wa kwanza kuunga mkono hadharani Umoja wa Afrika kujiunga na G20.