China kuendelea kufanya kazi na nchi wanachama wa G20 ili kukuza uchumi wa kidigitali duniani
2022-11-17 09:33:46| CRI

Rais Xi Jinping wa China amesema nchi yake itaendelea kufanya kazi na nchi wanachama wa kundi la G20 ili kukuza mtazamo wa uchumi wa kidijitali ulio na uwiano, wa kuratibiwa na kujumuisha wote, ambao unaleta manufaa kwa wote na kuangazia ushirikiano wa kunufaishana na ustawi wa pamoja.

Rais Xi amesema hayo alipohudhuria na kuhutubia mkutano wa 17 wa wakuu wa kundi la G20 kisiwani Bali, Indonesia.

Kwenye majadiliano kuhusu mabadiliko ya kidijitali, Xi alisema ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kasi ya mabadiliko ya kidijitali duniani kote yamekuwa mambo muhimu yanayoathiri hali ya uchumi wa dunia.

Amesema katika miaka ya hivi karibuni, kundi la G20 limejenga maelewano zaidi na kuongeza ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya kidijitali na kujenga uchumi wa kidijitali, akieleza matumaini yake kwamba pande zote zitaibua nguvu ya uhai katika ushirikiano wa kidijitali na kuleta manufaa ya uchumi wa kidijitali kwa watu wa nchi zote.

Ametoa wito kwa pande hizo kushikilia utaratibu wa pande nyingi na kuimarisha ushirikiano ili kukuza mazingira ya wazi, jumuishi, ya usawa, ya haki na yasiyo ya ubaguzi kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali, na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kukuza nyanja ya kidijitali na kukuza mageuzi ya kidijitali ya viwanda, ili kuibua uwezo wa uchumi wa kidijitali na kukuza maendeleo ya dunia. Alibainisha kuwa kujenga "yadi ndogo yenye uzio mrefu" na kupunguza au kuzuia ushirikiano katika sayansi na teknolojia kutaumiza maslahi ya wengine bila kujinufaisha, na kwamba vitendo hivyo haviendani na maslahi ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa.

Xi alisema ni muhimu kuweka maendeleo mbele na kuziba pengo la kidijitali. Pande hizo zinapaswa kuongeza mawasiliano katika enzi ya dijitali, na kuchukua hatua madhubuti za kukuza uwezo na ujuzi wa kidijitali kwa watu wote. Alisisitiza kuwa ni muhimu sana kusaidia nchi zinazoendelea na makundi nyonge kukabiliana na mabadiliko ya kidijitali na kujitahidi kuziba pengo la kidijitali.

Xi pia alitoa wito wa kufanywa juhudi kimataifa ili kutafuta maendeleo yanayopatikana kwa kutumia uvumbuzi na kuwezesha ufufukaji wa uchumi baada ya janga la COVID-19.

Azimio la mkutano wa wakuu wa kundi la G20 kisiwani Bali lilipitishwa katika mkutano huo.