Rais wa Uganda asema hatua zimechukuliwa ili kuzuia kuenea kwa Ebola
2022-11-17 09:35:09| CRI

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameihakikishia jumuiya ya kimataifa kwamba nchi hiyo imeweka mikakati ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa hatari wa Ebola.

Akilihutubia taifa moja kwa moja kupitia televisheni, Rais Museveni amesema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe na vituo vingine vya kuvuka mpaka wa nchi kavu vina vifaa vya kupima joto ili kuhakiki msafiri yeyote ambaye anaweza kuwa na ishara.

Rais amesema watu ambao wamewasiliana na watu wenye Ebola wamepigwa marufuku kusafiri, akiongeza kuwa majina yao yamepelekwa kwa maafisa wa uhamiaji. Amesisitiza kuwa kama watu hao hawatazingatia vizuizi vya serikali, na kutoroka kupitia mipaka ya nchi hiyo, majina yao yatapelekewa kwenye nchi jirani.

Museveni ametoa ufafanuzi huo baada ya wasiwasi kwamba watalii wa kigeni wameanza kufuta safari zao kwenda nchini humo. Hata hivyo amebainisha kuwa baadhi ya mikutano ya kimataifa imefutwa kwa sababu ya hofu ya kuenea kwa Ebola.