Xi asema China ni muungaji mkono thabiti wa mfumo wa kimataifa ambao kiini chake ni UM
2022-11-17 09:00:45| CRI

Rais Xi Jinping wa China amesema nchi inaunga mkono kithabiti mfumo wa kimataifa ambapo Umoja wa Mataifa ndio kiini chake.

Rais Xi alisema hayo jana Jumatano wakati alipokutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kando ya Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Kundi la G20 kisiwani Bali, Indonesia. Xi amebainisha kuwa ili kufikia amani duniani, madhumuni na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa lazima zizingatiwe na masuala halali ya usalama ya nchi zote yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito. Rais Xi alisema wakati dunia inashuhudia mabadiliko makubwa, ni muhimu kuweka mustakabali wa binadamu mbele na kufanya kazi kwa mshikamano ili kukabiliana na matatizo.

Pia alizitaka nchi kubwa kuwa mfano mzuri na kubeba jukumu la uongozi, ili kuleta imani zaidi na nguvu duniani. Sambamba na hayo ameeleza imani yake kwamba amani, maendeleo na ushirikiano wa kunufaishana vitasalia kuwa mwelekeo wa kihistoria usiozuilika na kwamba binadamu anafurahia mustakabali mzuri.