Siku ya kuzuia unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto
2022-11-18 08:00:34| CRI

Unyanyasaji wa watoto ni tatizo la kijamii ambalo huathiri afya ya akili ya wale wanaougua, inaweza kutokea kwa njia ya ndani ya familia au nje ya familia. Licha ya kuwepo tangu nyakati za kale, hivi karibuni lilitambuliwa kama tatizo kubwa la afya ya kijamii, lililopo duniani kote. Kwa kujua hilo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha rasmi azimio la kuiteua Novemba 18 kila mwaka kuwa Siku ya Dunia ya kuzuia na kuponya unyanyasaji wa kingono, ukatili na uonevu kwa watoto. Azimio hilo linazitaka nchi zote wanachama, mashirika husika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, viongozi wa dunia, waumini wa dini, mashirika ya kiraia, na wadau wengine husika kuadhimisha siku hii kila mwaka duniani kwa namna ambayo kila mmoja anaona inafaa zaidi.

Lakini mbali na kuadhimisha siku hii pia nchi na wadau mbalimbali wanapaswa kutoa ufahamu kwa umma juu ya watoto walioathiriwa na unyanyasaji wa kijinsia na haja ya kuzuia na kukomesha unyanyasaji wa kijinsia wa watoto, ukatili na uonevu. Kwa wale watakaobainika wanatekeleza vitendo dhidi ya watoto ni lazima wawajibishwe kikamilifu, kuhakikisha upatikanaji wa haki na tiba kwa waathirika na wahanga, pamoja na kuwezesha majadiliano ya wazi juu ya haja ya kuzuia na kuondoa unyanyapaa wao, kukuza uponyaji wao, kuthibitisha utu wao na kulinda haki zao. Hivyo leo hii kwenye kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake pia tutaangalia sula hili la unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto kwa mapana yake na kujua hatua mbalimbali zilizochukuliwa ili kuzuia.