China na Japan zafikia makubaliano ya kutuliza na kuendeleza uhusiano wa pande mbili
2022-11-18 10:04:33| CRI

Rais Xi Jiping wa China jana Alhamisi alikutana na waziri mkuu wa Japan Fumio Kishinda kando ya Mkutano wa 29 wa Viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC), na pande mbili zimefikia makubaliano matano ya kutuliza na kuendeleza uhusiano wa pande mbili.

Pande mbili zimekubaliana kuwa umuhimu wa uhusiano baina ya China na Japan haujabadilika na wala hautabadilika na pande zote zinatakiwa kufuata kanuni za nyaraka nne za kisiasa za China na Japan na kufuata makubaliano ya kisiasa kuwa nchi hizi mbili ni washirika na sio tishio. Pia wamekubaliana kuitisha duru mpya ya mazungumzo ya kiuchumi ya ngazi ya juu mapema, kuimarisha ushirikiano katika kuhifadhi nishati na ulinzi wa mazingira, maendeleo ya kijani, huduma za afya na uponyaji. Aidha wamekubaliana kufungua laini za simu za moja kwa moja za mifumo ya majini na angani chini ya idara za ulinzi mapema.

Wakati huohuo Xi amesema mwaka huu ikiwa nchi mbili zinaadhimisha kwa pamoja miaka 50 ya uhusiano kuwa wa kawaida, katika miongo mitano iliyopita zimepitisha nyaraka nne za kisiasa, kufikia maelewano mengi muhimu ya pamoja na kufurahia mabadilishano yaliyozaa matunda na ushirikiano katika maeneo mbalimbali.