WHO yasema Uganda itapata chanjo za majaribio za homa ya Ebola wiki ijayo
2022-11-18 10:12:26| CRI

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Uganda itapata chanjo za majaribio ya homa ya Ebola wiki ijayo, wakati nchi hiyo inajitahidi kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo unaosababisha vifo.

Mwakilishi wa WHO nchini Uganda Yonas Tegegn Woldemariam alitoa taarifa akisema kikundi cha kwanza cha watu watakaopata chanjo ni wale waliokuwa karibu na wagonjwa waliothibitishwa kuambukizwa homa ya Ebola na wahudumu wa afya wanaotibu wagonjwa. Aliongeza kuwa watu hao lazima waambiwe manufaa na madhara yanayoweza kutokea.

Kamanda anayeshughulikia mlipuko wa homa ya Ebola katika wizara ya afya ya Uganda Henry Kyobe alisema chanjo hizo zimefanyiwa majaribio hapo awali na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa binadamu.