Msomi wa Cameroon: Uungaji mkono wa China kwa Umoja wa Afrika kujiunga na G20 unatia moyo
2022-11-18 08:45:39| CRI

Sauti ya China kwenye Mkutano wa 17 wa Kilele wa Kundi la Nchi 20 (G20) uliofanyika kiswani Bali, Indonesia imefuatiliwa sana kwenye jumuiya ya kimataifa. Msomi wa Cameroon Dkt. Taling Tene Rodrigue alipohojiwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG), amesema, kauli aliyotoa Rais Xi Jinping wa China kwenye mkutano huo kuhusu kuuunga mkono Umoja wa Afrika kujiunga na Kundi la Nchi 20, inasisimua na kuzitia moyo nchi za Afrika, na kutoa ishara wazi ya kutoacha nyuma nchi yoyote kwenye maendeleo ya dunia.

Dkt. Taling Tene Rodrigue ambaye ni naibu mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Nchi Zinazotumia Lugha ya Kifaransa katika Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, amesema, idadi ya watu duniani imezidi bilioni nane, na hakuna nchi yoyote au mtu yeyote anayetakiwa kuachwa nyuma kwenye ustawi na utulivu wa dunia. Umoja wa Afrika kujiunga kwenye G20 kutaziwezesha nchi za Afrika kunufaika moja kwa moja kutokana na fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya mfumo wa G20. Amesema, China kuuunga mkono Umoja wa Afrika kujiunga na kundi hilo, kunadhihirisha jitihadi zinazofanywa na nchi hiyo katika kusukuma mbele maendeleo ya dunia yawe shirikishi zaidi, yawe na ustahimilivu zaidi, na yanufaishe wote.

Dkt. Rodrigue amesema, katika muda mrefu uliopita, China imetoa mchango mkubwa katika kuongeza sauti za nchi zinazoendelea kwenye usimamizi wa dunia. Kwa upande mmoja, China ikiwa ni nchi kubwa zaidi inayoendelea, maendeleo yake yenyewe yameinua kwa kiasi kikubwa ushawishi wa nchi zinazoendelea kwenye usimamizi wa dunia; na kwa upande mwingine, kwa kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo Umoja wa Mataifa, Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), BRICS na G20, China imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia ufuatiliaji wa nchi za Afrika, na kuchukua nafasi ya uongozi kwenye ushirikiano wa kimataifa na Afrika.