Maonyesho ya kidijitali ya Historia na Utamaduni ya Njia ya Hariri ya Baharini yafanyika Mombasa, Kenya
2022-11-22 14:54:45| CRI

Maonyesho ya Kidijitali ya Historia na Utamaduni ya Njia ya Hariri ya Baharini yenye jina la "Kusafiri tena kwa Njia ya Hariri” yaliyofadhiliwa kwa pamoja na Ubalozi wa China nchini Kenya na Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Kenya, yamefunguliwa kwenye Jumba la Makumbusho la Fort Jesus mjini Mombasa. Ofisa wa Utamaduni wa Ubalozi wa China nchini Kenya Bi. Zhou Meifen, na Mkurugenzi Msaidizi wa Makumbusho ya Taifa ya Kenya Bw. Asman Hussain wamehudhuria hafla hiyo.

Bi. Zhou Meifen amesema katika hotuba yake kwamba urafiki kati ya China na Kenya una historia ndefu. Mwanzoni mwa Enzi ya Ming,  Zheng He aliongoza meli zake katika safari saba za kwenda Magharibi, akitembelea nchi na kanda zaidi ya 30 ya Asia na Afrika, hadi kufika Malindi na Mombasa nchini Kenya, na kuweka historia ya "Njia ya hariri ya baharini". Jumba la Makumbusho la Fort Jesus linaonyesha idadi kubwa ya vyombo vya kauri vya China na mabaki mengine ya kitamaduni kutoka Njia ya Hariri ya Baharini, likishuhudia historia ya mawasiliano ya kirafiki kati ya China na Kenya.

Maonesho ya Historia na Utamaduni ya Njia ya Hariri ya Baharini yanayofanyika hapa ni urithi wa "moyo wa njia ya hariri " na yana umuhimu mkubwa katika kukuza mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na Kenya.

Bw. Hussain amesema maonesho hayo yanayofanyika katika Jumba la Makumbusho la Fort Jesus yana umuhimu wa kipekee, sio tu kwa mabadilishano ya kitamaduni, bali pia ni hatua muhimu ya kurithi urafiki wa kihistoria kati ya China na Afrika. Maonyesho hayo yanafuatilia historia ya Njia ya Hariri ya Baharini na kuongeza uelewa wa dunia hasa kuhusu China.

Hii ni mara ya kwanza kwa maonyesho ya kidijitali yenye mada ya "Njia ya hariri " kufanyika Afrika. Kazi mbili zilizoshinda kwenye Shindano la ubunifu wa Makumbusho ya "Njia ya hariri " pia zimeonyeshwa kwenye maonyesho hayo.