Mkuu wa ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika akutana na Kamishna wa Uchumi, Biashara, Viwanda na Madini wa Umoja wa Afrika
2022-11-22 14:52:57| CRI

Mkuu wa Ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika Balozi Hu Changchun amekutana na kamishna wa masuala ya Uchumi, Biashara, Viwanda na Madini wa Umoja wa Afrika Balozi Albert Muchanga.

Balozi Hu amesema urafiki kati ya China na Afrika una historia ndefu, na ujenzi wa jumuiya yenye hatma ya pamoja ya China na Afrika katika zama mpya umekuwa mfano wa kuigwa kwa ajili ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.

Chini ya mfumo wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika na pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja", China itafanya kazi na Afrika kupanua uuzaji wa bidhaa za Afrika kwenye soko la China, kufanyia uvumbuzi mbinu za kufadhili biashara, kupanua ushirikiano wa biashara ya mtandaoni wa Njia ya Hariri, na kuandaa shughuli kwa pamoja kama vile "Tamasha la Ununuzi la Bidhaa za Kiafrika", kuunga mkono ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama vile ujenzi wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, na kuhimiza maendeleo endelevu na yenye uwiano ya biashara kati ya China na Afrika.  

Balozi Muchanga amepongeza na kuitikia vyema mapendekezo ya ushirikiano aliyotoa Balozi Hu. Amesema viongozi wa China na Afrika wamesisitiza tena kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China CIIE, kwamba wataendelea kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana na kupata mafanikio kati ya Afrika na China, na upande wa Afrika una imani kubwa. Urafiki kati ya Afrika na China umeimarika zaidi kwa muda mrefu, na China ndiye mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika. Amesema Umoja wa Afrika unapenda kuzidisha ushirikiano na China katika nyanja mbalimbali za uchumi na biashara, na kutekeleza kwa pamoja matokeo ya mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika.