WFP yataka dola za kimarekani bilioni 1.27 ili kukabiliana na ukame katika Pembe ya Afrika
2022-11-23 08:05:40| cri

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) limesema linahitaji dola za kimarekani bilioni 1.27 katika miezi sita ijayo ili kukabiliana na ukame mbaya unaozikumba nchi tatu za Pembe ya Afrika.

WFP imesema ukame unaozikumba Kenya, Ethiopia na Somalia umesababisha uhaba wa chakula na hali mbaya ya utapiamlo, huku watu milioni 22 wakikabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula kutokana na ukame.

Shirika hilo limesema fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya shughuli zake zote katika nchi hizo tatu kuanzia mwezi Novemba mwaka 2022 hadi mwezi Aprili mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Shirika hilo, kanda ya Pembe ya Afrika inakabiliwa na tishio la njaa, huku utabiri ukionesha kuwa msimu wa mvua wa Oktoba mpaka Desemba huenda hautakuwa na mvua za kutosha, hali inayoonesha kuwa nchi hizo tatu zitakumbwa na ukosefu wa mvua kwa misimu mitano mfululizo.