Marais wa China na DRC wapeana salamu za pongezi kuadhimisha miaka 50 tangu nchi zao kurudisha uhusiano wa kawaida
2022-11-24 18:10:31| CRI

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) leo Alhamisi wamepeana salamu za pongezi kwa njia ya simu kuadhimisha miaka 50 tangu nchi zao kurudisha uhusiano wa kawaida.

Rais Xi ameeleza kuwa katika nusu karne iliyopita, uhusiano kati ya China na DRC umeendelea vizuri huku urafiki wao wa jadi ukiwa umeendelea kuimarika. Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa wenzi wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili uliojengwa katika msingi wa kushirikiana na kunufaishana umeshuhudia mazao tele halisi yanayozidisha ustawi wa watu wao. Amesema anazingatia sana maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili na anapenda kufanya juhudi pamoja na rais Tshisekedi katika kuhimiza hali ya kuaminiana kisiasa, kuimarisha ushirikiano wa ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa China na DRC kwa kutumia vyema fursa hii ya kuadhimisha miaka 50 tangu nchi hizo mbili kurudisha uhusiano wa kawaida.

Kwa upande wake Rais Tshisekedi amepongeza tena rais Xi kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC). Amesema kuwa anatarajia kuendeleza urafiki wa jadi na China na kusukuma mbele uhusiano wa wenzi wa kimkakati kati ya DRC na China upate mafanikio mapya na kuleta manufaa zaidi kwa watu wa nchi hizo mbili.