Jukwaa la Kikanda la wakulima wa Kusini mwa Afrika laipongeza Tanzania kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo
2022-11-25 11:49:56| CRI

Jukwaa la Kikanda la Wakulima wa eneo la Kusini mwa Afrika, limeipongeza serikali ya Tanzania kwa ongezeko kubwa la bajeti ya sekta ya kilimo na mpango wa kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Pongezi hizo zimetolewa mjini Dar es Salaam kwenye Mkutano wa Jukwaa hilo, na mkuu wa jukwaa hilo Bibi Elizabeth Nsimadala na Mwenyekiti Dkt Sinare Sinare kutokana na ongezeko la bajeti ya kilimo kwa zaidi ya asilimia 300. Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 za mwaka 2021/2022 hadi bilioni 954 mwaka 2022/2023, ambalo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 300.

Lengo kuu la Jukwaa hilo la Kikanda la Wakulima ni kuwakutanisha wakulima kupitia vikundi vyao, kujadili fursa na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kusaidia wakulima wadogo kuboresha maisha yao, kuimarisha usalama wa chakula na lishe na kupunguza umaskini vijijini.