Eneo la Tigray lapokea raundi ya kwanza ya msaada wa kibinadamu baada ya makubaliano ya amani kufikiwa
2022-11-28 09:04:18| CRI


 

Serikali ya Ethiopia imesema zaidi ya watu laki 4.5 walioko katika eneo la kaskazini la Tigray lililoathiriwa na mapambano, wamefikiwa katika raundi ya kwanza ya msaada wa kibinadamu baada ya makubaliano ya amani kusainiwa.

Kamisheni ya Usimamizi wa Hatari ya Majanga ya Ethiopia (NDRMC) imesema serikali ya Ethiopia imeimarisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu walio hatarini kwenye eneo hilo kupitia barabara nne na usafiri wa anga. Katika raundi hiyo ya kwanza, zaidi ya tani 9,000 za ngano na chakula cha lishe vimesambazwa.

Msaada huo umetolewa kufuatia pande hasimu kwenye eneo la Tigray kufikia makubaliano ya amani, na pia kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wote wenye mahitaji kwenye eneo hilo.