UM: korido za kibinadamu Tigray zimefunguliwa lakini bado hazitoshi
2022-11-29 09:08:10| CRI

Ofisi ya uratibu wa mambo ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema njia za misaada ya kibinadamu katika eneo la Tigray nchini Ethiopia zimefunguliwa tangu mapigano yasitishwe, lakini bado hazijakidhi mahitaji.

Ofisi hiyo imesema tangu katikati ya mwezi huu usambazaji wa misaada ulianza kuingia kwenye sehemu za kaskazini mwa Tigray, zikiwemo mji wa Mekelle, Semera na Kombolcha na sehemu nyingine kando ya ukanda wa Gondar katika jimbo la Amhara. Huduma za usafiri wa ndege za kibinadamu za Umoja wa Mataifa zimerejeshwa Mekelle na Shire.

OCHA pia imesisitiza kuwa misaada zaidi inahitajika. Zaidi ya watu milioni 5 wanahitaji msaada wa chakula na inakadiriwa kuwa asilimia 30 ya watoto wa eneo hilo watakabiliwa na utapiamlo mkali, na sasa ni muhimu kuhakikisha chakula na vifaa vingine vinavyohitajika vinawafikia wote wenye mahitaji huko Tigray.