China yatangaza wanaanga wa chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-15
2022-11-29 08:51:45| CRI


 

Shirika la anga za juu la China (CMSA) limetangaza wanaanga watatu watakaokuwa kwenye chombo cha anga za juu cha Shenzhou-15, kinachotarajiwa kurushwa leo. Wanaanga hao ni Fei Junlong, Deng Qingming na Zhang Lu, na kati yao Fei Junlong aliwahi kushiriki kwenye mradi wa Shenzhou-6, na wengine wawili ni wageni.

Msaidizi wa mkurugenzi wa Shirika la anga za juu la China Bw. Ji Qiming amesema hii ni safari ya sita na ya mwisho ya chombo cha anga za juu cha China kwa mwaka huu, na pia ni ya mwisho katika mchakato wa ujenzi wa kituo cha anga za juu cha China.

CMSA pia imetangaza kuwa miradi kadhaa ya maombi ya sayansi ya anga iliyochaguliwa kwa pamoja na China na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Anga za Juu au na Shirika la Anga za Juu la Ulaya inatekelezwa kama ilivyopangwa, na vifaa vinavyohusika vitarushwa ili kuingia kwenye kituo cha anga za juu cha China kwa ajili ya majaribio mwaka kesho. Idara hiyo pia imesema China itawakaribisha wanaanga kutoka nchi nyingine kuingia kwenye kituo chake cha anga za juu kufanya majaribio.