FAO yaongeza fedha ili kukabiliana na ukame katika maeneo ya vijijini Somalia
2022-11-30 09:01:05| CRI


 

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema limeongeza mwitikio wa kibinadamu kupitia utumaji wa fedha ili kupunguza athari za ukame kwa usalama wa chakula na maisha ya jamii za vijijini zilizoathirika nchini Somalia.

Mwakilishi wa FAO nchini Somalia Bw. Etienne Peterschmitt amesema ukame wa sasa unaoathiri nchi hiyo ni mkali zaidi kuwahi kutokea katika takribani miongo minne, na kuwa baadhi ya maeneo ya nchi yanakaribia kukumbwa na njaa.

Bw. Peterschmitt amesema utuimaji wa fedha kwa jamii za vijijini zilizo hatarini, unashughulikia mahitaji yao ya haraka na kusaidia kupunguza kuporomoka kwa maisha.

Kwa mujibu wa FAO takriban watu milioni 6.7, ikiwa ni pamoja na zaidi ya laki 3 ambao tayari wanakabiliwa na njaa, wanatarajiwa kukumbwa na uhaba wa chakula mwishoni mwa mwaka. Nusu yao ni wale walioko vijijini, walioko kwenye maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa, walioko kwenye maeneo yaliyoshindwa kuhimili ukame, na zaidi ya watu milioni moja ambao wameondoka makwao kwenda kutafuta msaada.