UM: Pembe ya Afrika inakabiliwa na dharura ya ukame
2022-11-30 09:00:33| CRI

Ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema Pembe ya Afrika inakabiliwa na dharura ya ukame yenye matokeo mabaya ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Kwenye taarifa yake ya hivi karibuni OCHA imesema hali ya ukame katika eneo la Pembe ya Afrika inaweza kuwa mbaya zaidi, kama hali ya hewa katika nchi zilizoathirika itazidi kuwa mbaya. 

Maeneo ya pembe ya Afrika yako kwenye msimu wa tano mfululizo bila mvua, ambapo mvua za kati ya Oktoba na Desemba 2022 zimeanza vibaya, hazinyeshi vya kutosha, na utabiri unaonyesha kuwa zinaweza kuendelea kuwa mbaya.

Takriban watu milioni 36.4 wa eneo la pembe ya Afrika, wanaathiriwa na ukame wa muda mrefu na mkali zaidi katika historia, ikiwa ni pamoja na milioni 24.1 waliopo nchini Ethiopia, milioni 7.8 nchini Somalia, na milioni 4.5 nchini Kenya.