Baraza la Usalama la UM lakaa kimya kwa dakika moja kuomboleza kifo cha Jiang Zemin
2022-12-02 09:08:56| CRI


 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatano lilikaa kimya kwa dakika moja ili kuomboleza kifo cha aliyekuwa rais wa China Jiang Zemin.

Mwenyekiti wa zamu wa Baraza hilo ambaye ni mjumbe wa kudumu wa Ghana katika Umoja wa Mataifa Balozi Harold Adlai Agyeman, amesema  Jiang Zemin alitoa mchango mkubwa katika kuhimiza mageuzi na ufunguaji mlango, ujenzi wa mambo ya kisasa na maendeleo ya uchumi nchini China, na vilevile amani, usalama na maendeleo ya dunia. Jumuiya ya kimataifa itamkumbuka Jiang Zemin kwa mchango wake, na kifo chake ni hasara kubwa kwa China na kwa jumuiya ya kimataifa.

Viongozi wa nchi mbalimbali na wa mashirika ya kimataifa pia wametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Jiang Zemin.

Rais Vladimir Putin wa Russia amsema komredi Jiang Zemin alitoa mchango muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya uchumi na jamii na kuinua hadhi ya kimataifa ya China. Amesema Jiang Zemin alikuwa ni rafiki mkubwa wa Russia, ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuinua uhusiano wa Russia na China uwe uhusiano wa wenzi wa kimkakati.

Rais wa Laos Thongloun Sisoulith amesema komredi Jiang Zemin alitoa mchango mkubwa katika kuendeleza ujamaa wenye umaalum wa China, alikuwa ni rafiki mkubwa wa Laos na watu wake, na aliongoza maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina amesema yeye na watu wa Palestina watamkumbuka daima kiongozi huyo hodari kwa kuwa yeye alikuwa ni muungaji mkono wa wapalestina na haki halali zao, mhimizaji wa uhusiano kati ya Palestina na China na pia shuhuda wa kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili.