Algeria na Jordan zasaini makubaliano matano ya kuimarisha uhusiano
2022-12-05 11:22:31| cri

Algeria na Jordan jana Jumapili huko Algiers zilitia saini makubaliano matano katika hafla iliyoongozwa na Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune pamoja na mgeni wake Mfalme Abdullah II wa Jordan aliyewasili Algiers Jumamosi jioni kwa ziara ya kiserikali kutokana na mwaliko wa Tebboune.

Makubaliano hayo yalijumuisha makubaliano ya maelewano kuhusu mashauriano ya kisiasa baina ya nchi hizo mbili, makubaliano ya msamaha wa viza kwa pande zote mbili kwa wenye pasipoti za kidiplomasia na makubaliano ya maelewano kati ya taasisi za kidiplomasia za nchi hizo mbili.

Nchi hizo mbili pia zilikubaliana kuanzisha mpango wa ushirikiano wa pamoja kati ya mashirika rasmi ya habari, na pande zote mbili kutambua vyeti stahiki vinavyotolewa kwa mabaharia na programu za mafunzo ya baharini.

Mapema jana, mawaziri wa Algeria na Jordan walifanya mazungumzo na kujadili njia za kukuza uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali, zikiwemo biashara.