Tanzania kuweka bango la Kiswahili kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro
2022-12-05 11:20:23| cri

Tanzania itaweka bango la Kiswahili kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, ambao ni mrefu zaidi barani Afrika, kama sehemu ya sherehe za kuadhimisha siku ya uhuru wa nchi hiyo zitakazofanyika tarehe 9 mwezi Desemba.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia James Mdoe amekabidhi bango hilo kwa timu ya wapanda milima mjini Dodoma.

Mdoe amesema wizara hiyo imepewa heshima ya kufundisha Kiswahili ndani na nje ya nchi, hivyo amesema kuna kila sababu ya kuenzi Kiswahili wakati wanapoadhimisha siku ya uhuru.

Kiswahili ni mojawapo ya lugha zinazotumiwa zaidi barani Afrika, ikijumuisha zaidi ya lahaja kuu kumi na mbili. Mlima Kilimanjaro ambao ni mojawapo ya vivutio vinavyoongoza vya utalii nchini Tanzania, upo takriban mita 5,895 kutoka usawa wa bahari. Takriban wasafiri 50,000 kutoka dunia kote wanajaribu kufika kilele cha mlima kila mwaka.