Maonyesho ya kilimo cha chakula ya Afrika yanaanza nchini Misri
2022-12-06 09:49:09| CRI

Maonesho ya saba ya kimataifa ya sekta ya chakula barani Afrika yamefanyika katika Kituo cha Maonyesho cha Kimataifa cha Cairo, nchini Misri, yakishirikisha zaidi ya waonyeshaji 700 kutoka zaidi ya nchi 30.

Maonyesho hayo yanalenga kutoa mtandao mzuri kati ya wafanyabiashara wa kimataifa na wachuuzi na wenzao kutoka Misri, Mashariki ya Kati, na kanda ya Afrika.

Maonyesho hayo yanayofanyika kwa siku tatu, yanapangwa kuwavutia wauzaji wa jumla, wasambazaji, wauzaji reja reja, na wataalamu wengine wa sekta hiyo ili kushughulikia mahitaji tofauti ya wanunuzi na waagizaji, pamoja na kuhudumia masoko mapya nchini Misri na Afrika.

Mmiliki wa kampuni ya usambazaji wa chakula kutoka Jordan Bw. Moatassem al-Hodob amesema wanatembelea maonyesho hayo kila mwaka kutafuta fursa mpya za biashara na kukutana na wasambazaji wapya ili kuona maendeleo mapya katika sekta ya kilimo cha chakula. Ameongeza kuwa amekutana na waonyeshaji kadhaa na atasaini mikataba kadhaa katika siku zijazo.

Mwakilishi wa kampuni ya al-Mona ya utengenezaji wa halva na tahini kutoka Saudi Arabia Bw. Mahmoud Abdel-Mohsen amesema anaweza kupata watoa huduma za malighafi kwenye maonyesho hayo huku akikutana na wanunuzi wapya.