UM yatafuta dola milioni 50 ili kusaidia watu laki 3.15 wenye uhitaji nchini DRC
2022-12-06 09:47:34| CRI

Shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa (UM) linatafuta karibu dola milioni 50 za kimarekani ili kusaidia watu laki 3.15 wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa Stephanie Tremblay, msemaji msaidizi wa katibu mkuu wa UM Antonio Guterres, katika jimbo la Kivu Kaskazini raia wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa mgogoro kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23. Amesema Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeripoti kuwa mapambano mapya yaliyoanza tangu mwezi Machi yamesababisha watu laki 3.9 kupoteza makazi yao, na wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Wengi wa watu waliokimbia makazi wanaishi na familia zinazowasitiri au kwenye maeneo ya watu walikosa makazi huko Rutshuru, Nyiragongo, Lubero, Masasi na mji wa Goma.

Bi Tremblay amesema OCHA na washirika wake wamewasaidia zaidi ya watu laki 1.3, kusambaza maji kwa mamia ya familia kwa siku, na watoto zaidi ya 1,500 wenye utapiamlo wamepata huduma zinazostahili.