Huawei yatoa mafunzo ya TEHAMA kwa wanafunzi nchini Ethiopia
2022-12-07 09:23:49| CRI

Kupitia Programu yake ya “Seeds for the Future”, kampuni kubwa ya teknolojia ya China Huawei imetoa mafunzo ya hali ya juu ya kubadilishana uzoefu kuhusu teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Ethiopia.

Programu hiyo iliyodumu kwa wiki moja, ilitoa mafunzo kwa wanafunzi 66 kutoka vyuo vikuu 12 vya Ethiopia. Mahafali ya kuhitimu mtandaoni yamefanyika mbele ya maafisa wa Wizara ya Elimu ya Ethiopia. Taarifa imesema wanafunzi wamejifunza kuhusu teknolojia ya kisasa na uvumbuzi kutoka kwa wahadhiri mashuhuri katika maeneo muhimu kama vile 5G, mitandao na wingu (cloud).

Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei nchini Ethiopia Bw. Chen Mingliang amesema fursa hiyo inasaidia kukuza vipaji vya vijana wa Ethiopia katika TEHAMA ili kusaidia mustakabali wa nchi hiyo.

Mkuu wa ICT na elimu ya kidijitali katika Wizara ya Elimu ya Ethiopia Bw. Zelalem Assefa amesema Huawei na Wizara hiyo zina historia ndefu ya kushirikiana katika programu hiyo. Afisa huyo pia ametoa pongezi zake kwa wanafunzi walioshiriki katika programu hii na kuipongeza Huawei kwa kusaidia kuinua vipaji vya vijana.