Makala inayosisitiza ushirikiano kati ya China na nchi za Kiarabu yachapishwa nchini Saudia
2022-12-08 09:32:20| CRI

Makala iliyoandikwa jina la  Rais Xi Jinping wa China imechapishwa leo Alhamisi kwenye gazeti la Saudi Arabia la Al Riyadh, wakati yupo nchini humo kuhudhuria Mkutano wa kwanza wa wakuu wa China na nchi za Kiarabu na Mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na nchi za Kiarabu za Ghuba (GCC), pamoja na kufanya ziara ya kiserikali mjini Riyadh.

Makala hiyo yenye kichwa cha "Kuendeleza Urafiki Wetu wa Milenia na Kujenga Mustakabali Bora kwa Pamoja", imegusia mambo makuu manne  kuhusu hali ya ushirikiano wa muda mrefu ambao umeanzia zaidi ya miaka 2000.  Rais Xi amesema, misafara ya mara kwa mara kati ya Njia ya Hariri ya nchi kavu na baharini imetoa ushuhuda wa jinsi ustaarabu wa China na nchi za Kiarabu ulivyoingiliana na kutiana moyo katika bara la Asia.

Akizungumzia suala la mshikamano na ushirikiano wa jumuiya ya China na nchi za Kiarabu  yenye mustakabali wa pamoja katika  zama mpya, Rais Xi amesema nchi za Kiarabu ni  nchi muhimu katika nchi zinazoendelea na ni nguvu muhimu ya kudumisha haki na uadilifu wa kimataifa.

Pia amegusia suala la juhudi za pamoja za kukuza ushirikiano wa kimkakati kati ya China na GCC, na  kuendelea na juhudi za kuleta ushirikiano wa kimkakati wa kina kati ya China na Saudi Arabia  kwenye viwango vipya.