Rais wa Tunisia aishukuru China kwa msaada wa muda mrefu wa maendeleo
2022-12-08 09:30:05| CRI

Rais wa Tunisia Kais Saied amepongeza ushirikiano kati ya Tunisia na China, na kutoa shukrani zake kwa msaada wa muda mrefu unaotolewa na China kwa ajili ya maendeleo ya Tunisia.

Wakati alipokutana na Balozi wa China ambaye atamaliza muda wake nchini Tunisia Bw. Zhang Jianguo, rais Saied amesema urafiki wa Tunisia na China una historia ndefu. Ameongeza kuwa fursa mpya za maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili zitajitokeza wakati wa kufanyika kwa Mkutano wa kwanza wa wakuu wa China na nchi za Kiarabu. Amesisitiza kuwa Tunisia inapenda kushirikiana na China ili kuimarisha na kuboresha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Pia alimshukuru balozi Zhang kwa mchango wake katika kuendeleza uhusiano wa nchi hizo mbili na urafiki kati ya watu wao.

Kwa upande wake, balozi Zhang amesema kuwa China na Tunisia zinaelewana na kusaidiana katika maslahi ya msingi na masuala ya pande zote. China inapenda kuungana mkono na Tunisia ili kuupandisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika ngazi mpya.