Zaidi ya watoto milioni 2.6 nchini Somalia wachanjwa dhidi ya polio na surua
2022-12-08 09:33:04| CRI

Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema watoto milioni 2.61 nchini Somalia wamechanjwa dhidi ya polio na surua.

Mashirika hayo yamesema kampeni jumuishi ya kitaifa ya chanjo ambayo ilianzishwa mwezi Novemba nchini Somalia inalenga watoto walio chini ya miaka mitano ili kuwaokoa na magonjwa yanayoweza kuzuilika kama vile polio na surua.

Mwakilishi wa WHO nchini Somalia Mamunur Rahman Malik amesema shirika hilo linatumia rasilimali zake zote zilizopo na mbinu za kiuvumbuzi kama vile kampeni jumuishi, matumizi ya nishati ya jua kwenye vituo vya afya ili kudumisha mnyororo baridi wa chanjo, na kushirikisha jamii ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto wa Somalia ambao wanastahili maisha mazuri na afya.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mzozo tatanishi wa kibinadamu unaosababishwa na migogoro, ukame wa muda mrefu, na watu kukimbia makazi yao nchini Somalia umeweka zaidi ya watoto milioni 3.6 chini ya miaka mitano hatarini.