Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Stephanie Tremblay amesema, vurugu katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini zimelazimisha watu wengi kukimbilia Sudan au kujificha katika vinamasi.
Bi Tremblay amesema, kwa mujibu wa waokoaji wa huko, asilimia 75 ya watu waliokimbia hivi karibuni ni wanawake na watoto, akibainisha kuwa ongezeko la kasi la idadi ya wakimbizi wapya limeleta shinikizo la ziada kwenye uwezo wa washirika wao kutoa huduma ya kuwasaidia wakimbizi hao.
Mratibu wa muda wa masuala ya kibinadamu wa Umoja huo nchini Sudan Kusini Bw. Peter Van der Auweraert, amelaani vikali vurugu hizo zinazoendelea na kusababisha watu zaidi ya elfu 9 kukimbia. Watu zaidi ya elfu 2.3 wamekimbilia hifadhi ya Malakal tangu mgogoro huo kuanza mwezi Agosti.