FAO yaongeza kutoa fedha za dharura kwa Somalia inayokumbwa na ukame
2022-12-09 09:31:17| CRI

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) jana lilisema limeongeza kutoa fedha za dharura ili kukabiliana na hali ya dharura katika maeneo ya vijiji vya Somalia yanayokumbwa na ukame mkali.

Kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari mjini Mogadishu, Mwakilishi wa FAO nchini Somalia Etienne Peterschmitt alisema kwa sasa mpango wa kuzuia njaa wa shirika hilo umepata asilimia 26 tu ya fedha zinazohitajika. Peterschmitt ameeleza kuwa kazi ya kuzuia njaa lazima ianze vijijini kwenye kitovu cha msukosuko, ambapo jamii zinazozalisha chakula zinaathiriwa zaidi na ukame.

Kwa mujibu wa FAO, watu takriban milioni 6.7 wa Somalia hawawezi kujikimu kimaisha, na watu zaidi ya laki tatu kati yao wanakabiliwa na baa la njaa. FAO pia ilisema kutoa fedha huenda ni chaguo zuri zaidi kuliko njia nyingine za utoaji wa msaada.