Xi ataka jumuiya ya China na nchi za Kiarabu yenye mustakabali wa pamoja kuwa ya karibu zaidi
2022-12-10 10:41:47| cri

Rais Xi Jinping wa China ametoa wito kwa China na nchi za Kiarabu kuendeleza moyo wa urafiki kati ya pande hizo mbili, na kukuza jumuiya ya China na nchi za Kiarabu yenye mustakabali wa pamoja kuwa ya karibu zaidi, wakati akihutubia kwenye Mkutano wa kwanza wa Wakuu wa China na Nchi za Kiarabu uliofanyika Ijumaa mjini Riyadh, Saudi Arabia.

Amesema China na nchi za Kiarabu zikiwa washirika wa kimkakati zinapaswa kuendeleza moyo wa urafiki kati yao, kuimarisha mshikamano na ushirikiano, na kuhimiza uhusiano wa karibu kati ya China na nchi za kiarabu wenye mustakabali wa pamoja, ili kunufaisha zaidi watu wao na kuhimiza maendeleo ya binadamu.

Ameongeza kuwa China na nchi za Kiarabu zinapaswa kujiamulia mambo wenyewe na kutetea maslahi yao ya pamoja, na kwamba China inaziunga mkono nchi za Kiarabu kutafuta wenyewe njia za maendeleo zinazoendana na hali zao za kitaifa na kushikilia kithabiti mustakabali wao mikononi mwao wenyewe.

Rais Xi amesema, China iko tayari kuongeza uaminifu wa kimkakati na nchi za Kiarabu, na kuunga mkono kithabiti katika kulinda mamlaka, ukamilifu wa ardhi na heshima ya taifa, akibainisha kuwa pande hizo mbili zinapaswa kushikilia kwa pamoja kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, kutekeleza kwa vitendo utaratibu wa pande nyingi, na kutetea haki halali na maslahi ya nchi zinazoendelea.

Rais Xi amesema China itashirikiana na nchi za Kiarabu kuendeleza mipango mikuu minane ya ushirikiano katika maeneo kama vile kuunga mkono maendeleo, usalama wa chakula, afya ya umma, uvumbuzi wa kijani, usalama wa nishati, mazungumzo kuhusu ustaarabu, maendeleo ya vijana, usalama na utulivu.