Watu 166 wauawa katika vurugu nchini Sudan Kusini
2022-12-16 07:57:28| CRI

Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema, watu 166 wameuawa na wengine 237 kujeruhiwa katika miezi minne iliyopita ya vurugu katika mkoa wa Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Katika taarifa yake, Turk amesema mauaji hayo pamoja na ripoti za ukatili wa kijinsia majumbani, utekaji nyara, uharibifu wa mali na uporaji ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na vinapaswa kukomeshwa. Ameitaka serikali ya Sudan Kusini kufanya uchunguzi wa wazi usio na upendeleo na wa haraka kuhusu vurugu hizo na kuwafikisha wahusika wote mbele ya sheria. Pia amewataka viongozi wa kijamii na wazee kutumia ushawishi wao kwa makundi yanayohusika katika vurugu hizo kuacha vitendo hivyo vya umwagaji damu.

Tangu mwezi Agosti, mkoa wa Upper Nile nchini Sudan Kusini umeshuhudia mapigano ambayo pia yalisababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.