Argentina yatwaa kombe la dunia baada ya kuichapa Ufaransa kwa mikwaju ya penalti
2022-12-19 08:55:08| CRI

Argentina imetwaa kombe la dunia baada ya kuifunga Ufaransa kwenye mikwaju ya penalti baada ya fainali kati ya timu hizo mbili kuisha kwa sare ya magoli 3-3 katika muda wa dakika 120.

Argentina ilitangulia kwa mabao mawili katika kipindi cha kwanza, ni Lionel Messi alikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 23 kwa mkwaju wa penalti baada ya Ousmane Dembele kumwangusha Ángel Di María katika eneo la hatari, na Di maria aliifungia timu yake bao la pili dakika ya 36 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Alexis Mac Allister.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alifanya mabadiliko katika kipindi cha pili kwa kuwatoa Dembele na Olivier Giroud, na kuwaingiza Marcus Thuram na Randal Kolo Muani, mabadiliko ambayo yalifanya Ufaransa kusawazisha magoli mawili kupitia mshambuliaji wake Kilian Mbappe

Katika dakika za 80 na 81.

Katika muda wa nyongeza Lionel Messi aliweka mpira wavuni katika dakika ya 108, na baadaye Mbappe alisawazisha kwa penalti katika dakika ya 118.

Baada ya kupigiana Penalti, Argentina waliibuka washindi kwa penalti 4-2 baada ya Kingsley Coman na Aurelien Tchouameni wa Ufaransa kukosa penalti zao.