Zanzibar yaandaa kongamano la 6 la kimataifa la Kiswahili
2022-12-19 08:53:48| CRI

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi jana alifungua kongamano la 6 la kimataifa la Kiswahili na kuwataka washiriki kuifanya lugha hiyo kuwa ya kimataifa.

Akiongea kisiwani Pemba linakofanyika kongamano hilo, Dk. Mwinyi amewataka wajumbe hao kutoka sehemu mbalimbali duniani kuunga mkono juhudi zinazolenga kudhihirisha umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa Zanzibar, Tanzania na dunia kwa ujumla.

Dk. Mwinyi amekumbusha kuwa Kiswahili kina nafasi kubwa ya kuwa na mchango katika maendeleo ya uchumi na uwezeshaji wa watu binafsi, kwani walimu watapata ajira ya kufundisha lugha hiyo katika nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini na katika nchi saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Pia amesema nchi mbalimbali zinatumia lugha ya Kiswahili katika matangazo ya redio na televisheni, na kufundisha lugha hiyo katika vyuo vyao vya elimu ya juu, jambo ambalo pia ni fursa nyingine kwa watanzania kupata ajira.