Spika wa bunge la Iran asema Marekani inatumia vikwazo kama nyenzo ya kushinikiza nchi nyingine
2022-12-19 08:54:28| CRI

Spika wa bunge la Iran Bw. Mohammad Baqer Qalibaf amesema Marekani inatumia vikwazo kama njia ya kushinikiza nchi yoyote inayokwenda kinyume na maoni yake.

Kwenye mazungumzo kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nicaragua Bw. Denis Moncada aliyeko ziarani mjini Tehran, Bw. Qalibaf ametoa wito wa kuwepo ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja za uchumi, kilimo, nishati na teknolojia.

Spika huyo pia ameisisitiza umuhimu wa kuboreshwa uhusiano wa pande mbili kwa ajili ya kulinda maslahi ya nchi zote mbili, na kusema ushirikiano kati ya nchi zao ni muhimu hasa kwa kuwa zote mbili zinakabiliwa na vikwazo vikali vya Marekani.

Bw. Moncada amesema ziara yake nchini Iran ni ishara ya juhudi zinazoendelea za nchi hizo mbili,  kuendeleza uhusiano na kuongeza uungaji mkono kati yao dhidi ya maadui wa pamoja.