UM wazindua mpango wa mwitikio wa kibinadamu wa Sudan Kusini kwa mwaka 2023
2022-12-21 08:51:26| CRI

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema mpango wa mwitikio wa kibinadamu wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.7 kwa ajili ya Sudan Kusini umezinduliwa ili kuwasaidia watu milioni 6.8 walio hatarini zaidi katika mwaka ujao.

Bw. Dujarric amesema kampeni ya mwaka kesho inalenga kuwasaidia wahanga wa migogoro, mabadiliko ya tabia nchi, na wale waliohama kwa muda mrefu. Akimnukuu mratibu wa masuala ya kibinadamu kuhusu Sudan Kusini Bibi Sara Nyanti, Bw. Dujarric amesema wakati mgogoro wa Sudan Kusini unashindana na dharura nyingine za kimataifa na kupungua kwa ufadhili, watu wa Sudan Kusini wanastahili msaada zaidi na sio tu juhudi zinazowawezesha kuendelea kuishi.

Amesema Bibi Nyanti pia amesisitiza haja ya wafanyakazi wa utoaji wa misaada kuwafikia kwa usalama na bila vizuizi wale wote wanaohitaji.

Zaidi ya theluthi mbili ya wakazi wa Sudan Kusini watahitaji aina fulani ya msaada wa kibinadamu na ulinzi kwa mwaka 2023.