Idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula kutokana na ukame nchini Kenya yaongezeka
2022-12-21 08:49:35| CRI

Kenya imesema idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula nchini humo huenda ikaongezeka kutoka milioni 4.3 wa sasa kutokana na ukame unaoendelea.

Ofisa mkuu mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Ukame (NDMA) Bw. Hared Adan, amesema mjini Nairibi kuwa mvua zinazoripotiwa zinatarajiwa tu kuongeza vyanzo vya maji na kufufua malisho katika maeneo yenye ukame na ardhi nusu kame (ASAL), lakini majira ya kiangazi ya Januari hadi Machi 2023 huenda yakabadilisha ahueni yoyote inayoshuhudiwa sasa.

Bw. Adan pia amesema matatizo ya ukame huenda yakaongezeka tena mwaka kesho, kwa hiyo mwitikio wa dharura wa ukame unahitajika, kwenye kaunti 13 ambazo ziko katika hatua ya tahadhari huku nyingine saba zikiwa katika awamu ya hatari ya ukame.

Pia amesema moja ya athari kuu za ukame ni vifo vya mifugo vinavyokadiriwa kufikia milioni 2.5 katika kaunti zenye ukame.