Makampuni ya China nchini Uganda yameimarisha uhusiano kati ya wenyeji na wachina
2022-12-22 08:55:02| CRI

Makampuni ya China nchini Uganda yanazidisha uhusiano kati ya wenyeji na wachina kupitia kazi za wajibu kwa jamii zinazofanywa na mashirika hayo.

Ripoti ya “Wajibu wa Kijamii wa Makampuni ya China kwa mwaka 2022," iliyozinduliwa jumanne mjini Kampala na Makamu wa Rais wa Uganda Bibi Jessica Alupo, ilifanya tathmini ya makampuni 21 kati ya 129 wanachama wa Chama cha Wafanyabiashara wa China nchini Uganda, na kuonesha kuwa makampuni hayo yamesaidia jumuiya za wenyeji kwa kutoa kambi za matibabu, ufadhili wa masomo, ujuzi na mafunzo, na ukarabati wa shule.

Bibi Alupo amesema China inaendelea kuchukua nafasi muhimu katika kuharakisha maendeleo ya Uganda, hasa katika sekta za uchukuzi na miundombinu ya nishati. Amesema China imefadhili ujenzi wa mitambo miwili mikubwa ya kufua umeme wa maji nchini Uganda, na sasa inashiriki katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe. Pia amesema China imepanua uingiaji wa bila ushuru wa hadi asilimia 98 ya bidhaa za Uganda kwenye soko la China.

Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong amesema kufuatia Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika mwaka jana nchini Senegal, miradi zaidi itatekelezwa ili kuboresha moja kwa moja maisha ya jamii za huko.