Ethiopia yafanikisha kuachiwa kwa wanajeshi 6 wa Djibouti waliotekwa nyara
2022-12-22 08:56:52| CRI

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema imefanikisha kuachiwa kwa amani kwa wanajeshi sita wa Djibouti waliotekwa nyara na kundi la waasi wenye silaha la FRUD (Front for the Restoration of Unity and Democracy) wakati wa shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi mwezi Oktoba mwaka huu, shambulizi ambalo pia lilisababisha vifo vya wanajeshi wengine saba.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, wizara hiyo imesema serikali ya Ethiopia imefanikisha kuachiwa huru kwa wanajeshi hao wa Djibouti kupitia hatua makini za ujasusi na operesheni za polisi, pamoja na mbinu za jadi za msaada kutoka kwa serikali ya Mkoa wa Afar wa Ethiopia na wazee wa eneo hilo. Taarifa imesema wanajeshi sita wa Djibouti tayari wamekabidhiwa kwa serikali ya Djibouti.

Shambulizi la silaha dhidi ya kambi ya jeshi la Djibouti lililaaniwa na serikali nyingi, pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa.