UM wasema kuendelea na mazungumzo na Burkina Faso baada ya afisa mkuu kufukuzwa
2022-12-26 08:54:21| CRI


 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametoa taarifa akisema Umoja wa Mataifa umenuia kuendelea kushirikiana na serikali ya Burkina Faso baada ya afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa kutangazwa kama "mtu asiyekubaliwa na kukaribishwa" na mamlaka ya nchi hiyo.

Bw. Dujarric amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres "amepokea habari hizo kwa masikitiko" baada ya serikali ya mpito ya Burkina Faso kumtangaza Barbara Manzi, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini humo, kama "mtu asiyekubaliwa na kukaribishwa,"

Serikali ya Burkina Faso siku ya Ijumaa ilitoa tamko hilo na kumtaka Manzi kuondoka nchini humo mara moja.

Hata hivyo kwenye taarifa yake Dujarric amesisitiza kuwa tamko kama hilo la kumtaja "mtu asiyekubaliwa na kukaribishwa" halitumiki kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa. Chini ya Ibara ya 100 na 101 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaoteuliwa na Katibu Mkuu, wanawajibika na umoja huo pekee, na Katibu Mkuu pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuamua, baada ya uchunguzi wa kina, kuhusiana na kujiondoa kwa afisa yeyote wa Umoja wa Mataifa.