Ujumbe wa serikali ya Ethiopia waenda mji mkuu wa Tigray unaodhibitiwa na waasi
2022-12-27 09:35:26| CRI


 

Ujumbe wa maafisa wa serikali kuu nchini Ethiopia Jumatatu ulikwenda Mekele, mji mkuu wa eneo la Tigray unaoshikiliwa na waasi nchini humo.

Safari hiyo iliyokuja baada ya makubaliano ya kusitishwa moja kwa moja kwa uhasama, ambayo yalitiwa saini Novemba 2 kati ya serikali ya Ethiopia na Chama cha Tigray TPLF, ambacho sasa kinadhibiti eneo la kaskazini mwa nchi, ni ya kwanza kwa ujumbe huo wa serikali tangu mzozo uzuke mwezi Novemba mwaka 2020.

Kwenye taarifa yake, Huduma ya Mawasiliano ya Serikali ya Ethiopia ilisema ujumbe huo, ukiongozwa na spika wa Baraza la Wawakilishi la Watu wa Ethiopia, Tagesse Chafo, unatarajiwa kusimamia utekelezaji wa vifungu muhimu katika makubaliano ya amani.

Mapema mwezi uliopita, pande mbili za mgogoro wa Ethiopia zilikubaliana rasmi kusitisha mapigano na kupokonywa silaha kwa utaratibu. Makubaliano hayo pia yanajumuisha kurejesha sheria na utulivu, kurejesha huduma, na upatikanaji usio na vizuizi wa vifaa vya kibinadamu.