Idadi ya vifo kutokana na pombe feki yafikia 92 nchini India
2022-12-28 08:47:00| CRI


 

Mwezi huu umeshuhudia takriban watu 90 wakifariki na wengine wengi kulazwa hospitalini baada ya kunywa pombe kali ya kughushi katika jimbo la mashariki mwa India la Bihar.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo, vifo hivyo vilitokana na uuzaji wa pombe feki katika jimbo hilo, ambapo kwa mujibu wa sheria uuzaji na unywaji wa vileo ni marufuku kabisa. Awali vifo hivyo viliripotiwa kutokea katika wilaya ya Saran. Kwa mujibu wa maafisa, wahanga walikuwa wamenunua pombe hiyo kisiri kutoka kwa wauzaji ambao hawakuidhinishwa waliokuwa wakitengeneza pombe hiyo kienyeji. Baada ya kunywa, walilalamika kuhisi kizunguzungu, kutapika na kutoona vizuri.

Ingawa walipelekwa hospitalini mara moja, wengi wao walikufa na wengine wengi kuripotiwa kupofuka. Taarifa kama hizo pia zilipokelewa kutoka maeneo ya jirani na wilaya. Kwa mujibu wa redio ya taifa ya India All India Radio (AIR), idadi ya waliofariki katika tukio hilo imeongezeka hadi 92.