Marais wa China na Benin wapongezana kwa kutimiza miaka 50 tangu nchi hizo zirejeshe uhusiano wa kibalozi
2022-12-30 09:13:19| CRI


 

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Benin Patrice Talon, wametumiana salamu za pongezi ili kuadhimisha miaka 50 tangu nchi hizo mbili zirejeshe uhusiano wa kibalozi.

Kwenye salamu zake rais Xi amesema katika nusu karne iliyopita, China na Benin zimedumisha urafiki wa dhati, na kuungana mkono katika masuala yanayohusisha maslahi yao makuu na yale muhimu yaliyofuatiliwa na nchi hizo mbili. Ameongeza kuwa hivi sasa uhusiano kati ya China na Benin unaendelea vizuri, na ushirikiano wao katika sekta mbalimbali umepata matokeo makubwa, na kuleta manufaa halisi kwa watu wa nchi hizo mbili. Rais Xi amesisitiza kuwa anatilia maanani sana maendeleo ya uhusiano kati ya China na Benin, na kupenda kushirikiana na rais Talon kukuza zaidi ushirikiano wa nchi hizi mbili katika sekta zote kufuatia pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, na kuhimiza uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuwa wa kiwango cha juu zaidi.

Kwa upande wake, Rais Talon ameeleza kuridhika na ushirikiano wenye mafanikio halisi kati ya Benin na China katika miaka 50 iliyopita, na kupenda kushirikiana na rais Xi kuanzisha uhusiano imara na wenye uhai zaidi kati ya nchi hizo mbili.