Kiongozi wa kikosi cha Iraq asema mauaji yaliyofanywa na Marekani yamefanya kuondoka kwa majeshi ya kigeni kuwa lazima
2022-01-03 08:58:07| CRI

Mkuu wa kikosi cha Hashd Shaabi cha Iraq Bw. Falih al-Fayadh, amesema shambulizi la anga la Marekani lililowaua kamanda wa Iran Qassem Soleimani na naibu mkuu wa kikosi cha wanamgambo cha Hashd Shaabi Abu Mahidi al-Muhandis, yamethibitisha ulazima wa kuondoa majeshi ya kigeni kutoka Iraq.

Al-Fayadh amesema hayo katika maandamano yaliyofanywa na waungaji mkono wa Hashd Shaabi katika uwanja wa ndege wa Baghdad, huku akisisitiza kuwa mauaji hayo yameonesha uhalisia mpya kwamba mahitaji ya kuondoa majeshi ya kigeni nchini humo hayawezi kuahirishwa.

Maandamano hayo yamefanyika miaka miwili baada ya shambulizi la droni lililofanywa na Marekani dhidi ya msafara wa magari karibu uwanja wa ndege wa Baghdad, na kusababisha vifo vya Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis. Shambulizi hilo limeleta hali ya wasiwasi na mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya Iran na Marekani nchini Iraq.

Bunge la Iraq lilipitisha azimio linaloitaka serikali kukomesha uwepo wa vikosi vya kigeni nchini humo siku mbili baada ya shambulizi hilo kutokea.