Taarifa ya pamoja ya nchi tano zenye silaha za nyuklia yatajwa kuwa italinda utulivu wa kimkakati duniani
2022-01-04 08:47:13| CRI

Viongozi wa nchi tano zenye silaha za nyuklia ambazo ni China, Russia, Marekani, Uingereza na Ufaransa jana Jumatatu walitoa taarifa ya pamoja kuhusu kuzuia vita vya kinyuklia na kuepusha mashindano ya silaha. Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Ma Zhaoxu alipohojiwa na wanahabari amefafanua umuhimu wa taarifa hiyo, na juhudi ilizofanya China, pamoja na mapendekezo ya China kuhusu kuimarisha usimamizi wa silaha za nyuklia duniani.

Bw. Ma amesema taarifa hiyo ya pamoja imesisitiza kuwa vita vya nyuklia havitakuwa na mshindi na wala havitakiwi kutokea, na nchi hizo tano hazitalenga silaha zao za nyuklia dhidi ya upande wowote mwingine kati yao au nchi nyingine. Anaona hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa nchi hizo tano kutoa taarifa ya pamoja kuhusu suala la silaha za nyuklia, ambayo imeonesha nia yao ya kisiasa ya kuzuia vita vya nyuklia, na pia imetoa sauti ya pamoja ya kulinda utulivu wa kimkakati duniani na kupunguza hatari ya kutokea kwa mapambano ya kinyuklia.