Nchi 5 zachukua majukumu ya ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
2022-01-05 09:06:28| CRI

Albania, Brazil, Gabon, Ghana na Umoja wa Falme za Kiarabu, zimeanza majukumu ya wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Muda rasmi wa ujumbe wa nchi hizo ni miaka miwili kuanzia januari 1, lakini kutokana na mapumziko ya sikukuu za Krismas na mwaka mpya, nchi hizo zimeanza kutekeleza majukumu yao Jumanne, na sherehe ya kupandisha bendera za nchi hizo pia ilifanyika.

Balozi wa Kazakhstan kwenye Umoja wa Mataifa Bw. Magzhan Ilyassov aliyeendesha shughuli ya kupandisha bendera, amezipongeza nchi hizo wajumbe wapya, na kuzitakia mafanikio katika kufanikisha vipaumbele vyao katika kipindi chao cha miaka miwili.

Amesema wanaamini kuwa mwaka huu ni mwaka wa matumaini kwa wote na kwa Umoja wa Mataifa. Pia amesema amani, usalama na maendeleo endelevu ya dunia, vitategemea maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mfumo wa umoja wa mataifa na wadau wengine.