Mwanzoni mwa mwaka mpya, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi ambaye pia ni mjumbe wa taifa wa China ametembelea nchi tatu za Afrika, ambazo ni Eritrea, Kenya na Comoro.
Huu ni mwaka wa 32 mfululizo kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa China kufanya ziara ya kwanza ya mwaka mpya katika nchi za Afrika, hali inayodhihirisha kuimarika zaidi kwa urafiki kati ya China na Afrika zaidi kadiri muda unavyopita, na ushirikiano kati ya pande hizo mbili utaendelea kwa kina na upana.
Desturi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China kufanya ziara yake ya kwanza ya mwaka barani Afrika imedumishwa kwa miaka 32 tangu mwaka 1991. Katika miaka 32 iliyopita, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China wamebadilika, lakini desturi hiyo nzuri haijabadilika. China ndiyo nchi kubwa zaidi inayoendelea, na Afrika ndilo bara lenye nchi nyingi zaidi zinazoendelea. Kuimarisha na kuendeleza mshikamano na ushirikiano na nchi za Afrika ni sera thabiti ya kimkakati ya kidiplomasia ya China. Bila kujali mabadiliko ya hali ya kimataifa, na maambukizi ya janga la COVID-19, China haitalegeza nia yake ya kuendeleza mawasiliano ya kirafiki na Afrika, na kuimarisha uungaji mkono wake kwa nchi za bara hilo. Hii pia ni tafsiri bora zaidi ya ahadi ya China ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja kati ya pande hizo mbili katika enzi mpya.
Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ulifanyika mwishoni mwa mwezi Vovemba mwaka jana nchini Senegal. Katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais Xi Jinping wa China alitangaza “Miradi Tisa” ya ushirikiano kati ya China na Afrika, ambayo ilipongezwa sana na nchi za Afrika, na kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa kushirikiana kati ya pande hizo mbili. Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, pande hizo mbili zilianza haraka mchakato wa utekelezaji wa matokeo yaliyopatikana, na hadi sasa mafanikio ya awali yameonekana. Kwa mfano, zaidi ya mwezi mmoja baada ya mkutano huo, China imetoa dozi milioni 6.8 za chanjo ya COVID-19 kwa nchi tisa za Afrika zikiwemo Zimbabwe na Msumbiji, na kundi la kwanza la “Vituo vya Vielelezo vya Teknolojia za Kilimo vya China na Afrika” pia vimeanzishwa.
Wang ametembelea tena Afrika zaidi ya mwezi mmoja baada ya kuhudhuria mkutano huo, akiwa na lengo la kuhimiza utekelezaji wa matokeo ya mkutano huo. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, ziara ya Wang ilikuwa na malengo makuu mawili. Kwanza ni kuhimiza utekelezaji wa ahadi ya China ya kuipatia Afrika dozi nyingine bilioni 1 za chanjo ya COVID-19 iliyotangazwa kwenye mkutano huo, na kuharakisha upatikanaji wa chanjo za kutosha barani Afrika, ili kuisaidia Afrika kufikia lengo la kuchanja asilimia 60 ya watu barani Afrika mwaka huu. Pili ni kuunga mkono nchi alizotembelea kutekeleza hatua mpya za ushirikiano, kusikiliza maoni na mapendekezo ya nchi hizo, na kuhimiza utekelezaji wa “Miradi Tisa” na makubaliano mengine yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Dakar, ili kupata mafanikio mapema, na kuzisaidia nchi hizo kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto kutokana na janga la COVID-19.
Ziara hiyo ya Wang barani Afrika katika mwaka mpya bila shaka imeleta mwanzo mzuri kwa ushirikiano kati ya China na Afrika. Tunaamini kuwa uhusiano wa kushirikiana kati ya pande hizo mbili utaendelea kukua zaidi katika siku zijazo.