Msomi wa Nigeria: Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China barani Afrika yathibitisha mara nyingine kuwa China ni rafiki wa kweli kwa Afrika
2022-01-11 09:30:18| CRI

Msomi wa Nigeria: Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China barani Afrika yathibitisha mara nyingine kuwa China ni rafiki wa kweli kwa Afrika_fororder_2129828852

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Nigeria cha Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang Dkt. Michael Ehizuelen amesema, ziara ya kwanza ya mwaka mpya ya Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi barani Afrika iliyofanyika katika kipindi ambacho janga la Corona bado linaendelea kusambaa kote duniani, ikiwa ni mwaka wa 32 kwa mawaziri wa mambo ya nje wa China kuenzi desturi hii, imethibitsha mara nyingine tena kwamba China ni rafiki wa kweli wa Afrika katika dhiki na faraja.

Dkt. Ehizuelen amesema, kati ya nchi zote kubwa zilizoahidi kuisaidia Afrika kupambana na janga la Corona na kufufua uchumi, ni waziri wa mambo ya nje wa China tu ndiye amechagua kufanya ziara yake ya kwanza katika mwaka mpya barani Afrika, desturi hiyo maalumu ambayo imeenziwa kwa zaidi ya miaka 30 mfululizo, inaonesha kuwa China inatilia maanani sana uhusiano kati yake na Afrika. Amesema, nia thabiti na ahadi ya China ya kudumisha mawasiliano ya kidiplomasia na nchi za Afrika daima inathaminiwa na watu wa Afrika, ikiwa ni sifa isiyolinganishwa na washirika wengine wa Afrika.

Dkt. Ehizuelen anaona, mawaziri wa mambo ya nje wa China wa awamu zote walipotembelea bara la Afrika, walifuatilia masuala matatu muhimu ambayo ni kutokomeza ukoloni, ushirikiano wa kunufaishana na maendeleo ya Afrika, na wote walisisitiza umuhimu wa kuimarisha majadiliano na uratibu kati ya China na Afrika kwenye mambo ya kimataifa, kwani viongozi wa China wanaamini kuwa, ni majadiliano ndiyo yanayoleta maendeleo. Dkt. Ehizuelen amesema, tofauti na nchi za magharibi, viongozi wa China siku zote wanafuata ahadi zao na kudumisha mwendelezo wa sera kwa Afrika, hali ambayo imeifanya China kuwa “rafiki wa hali zote” anayetegemeka kwa Afrika.  

Dkt. Ehizuelen amebainisha kuwa, Afrika ni bara ambalo idadi ya watu inaongezeka kwa kasi na linahitaji uwekezaji mkubwa, na viongozi wake mara kwa mara wameisifu China kwa kuzitendea kwa sawa nchi za Afrika. Mikutano ya kila baada ya muda kati ya viongozi wa China na Afrika imethibitisha kuwa nguvu ya uhusiano kati ya pande hizo mbili inatokana na urafiki, mshikamano, kuaminiana na kuheshimiana, vitu ambavyo vimetia uhai kwenye uhusiano wao, kuhimiza maendeleo endelevu ya pande mbili na kuchangia kwenye ujenzi wa Jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja katika zama mpya.

Dkt. Ehizuelen anaona, ziara hii ya Bw. Wang Yi itasukuma mbele zaidi maendeleo yenye ubora kwenye ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kati ya China na Afrika katika kipindi cha baada ya janga la Corona, na kujenga “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kuwa njia ya ushirikiano inayokabiliana na changamoto kwa pamoja, njia ya afya inayolinda afya ya umma, njia ya ufufukaji inayohimiza ufufukaji wa uchumi na jamii, na vilevile njia ya ukuaji inayozisaidia nchi za Afrika na China kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo.