Zanzibar yaadhimisha miaka 58 ya mapinduzi
2022-01-13 08:31:14| CRI

Tanzania Zanzibar jana iliadhimisha miaka 58 ya mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa Kisultani na serikali ya kiarabu yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Sherehe hizo zilizofanyika katika Uwanja wa Amaan visiwani Unguja, ziliongozwa na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Zikiwa na kaulimbiu ya “Uchumi wa Bluu kwa Maendeleo Endelevu,” sherehe hizo zilipambwa na maonyesho ya kijeshi yaliyoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Tanzania (TPDF) na dansi za asili za makabila mbalimbali.

Akihutubia kwa njia ya televisheni usiku wa jumanne, rais Mwinyi alisema, pamoja na mambo mengine, Zanzibar imepokea miradi 120 ya uwekezaji yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 787 kati ya mwezi Novemba 2020 na Desemba 2021, ambayo inakadiriwa kutoa nafasi 7000 za ajira kwa Wazanzibari.