Jeshi la Burkina Fasao limetangaza kumwondoa madarakani Rais Roch Marc Christian Kabore na kuvunja serikali, bunge na kufunga mipaka ya nchi hiyo.
Kabla ya hapo chama tawala cha nchi hiyo kilitoa taarifa ikisema rais Kabore ameokolewa katika jaribio la mauaji. Taarifa imesema uasi uliofanywa na baadhi ya wanajeshi umeendelea na kuelekea kuwa mapinduzi ya kijeshi.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres ametoa wito watendaji wote nchini Burkina Faso wajizuie na kufanya mazungumzo. Bw. Guterres amelaani vikali jaribio lolote la kutwaa serikali kwa njia ya kisilaha, huku akitoa wito kwa viongozi wa mapinduzi kuweka chini silaha.
Wakati huohuo, mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Faki Mahamat pia amelaani jaribio la mapinduzi nchini Burkina Faso, akisema anafuatilia hali mbaya ya nchini humo.